Lugha ya Kimakonde inazungumzwa na watu zaidi ya milioni moja na nusu hasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, kusini mwa Tanzania, na pia katika mikoa ya kaskazini mwa Msumbiji. Madhumuni ya kamusi hii ni kuwafikia wazungumzaji wa lugha hii na hivyo kutoa mchango katika kuikuza na kuihifadhi. Ni matumaini yetu kuwa mchango huu utatoa changamoto kwa Wamakonde kutaka kuiboresha kamusi hii na kuitumia kuwafunza vijana matumizi makini ya lugha yao. Pia tunatumaini kwamba wazungumzaji wa lugha nyingine nyingi za Tanzania ambazo hazina maandiko yoyote watahamasika na kuanza kazi ya kuziandika lugha hizi.








